Menu

About Publisher
Ukurasa Wa Mbele
Nyakati Duniani
Habari Mbalimbali
Barua za Wasomaji
Kauli Ya Mhariri
Makala 
Mjadala
Matangazo 
Bible Study
Tuwasiliane 
GuestBook Page

WWW.NYAKATI.FAITHWEB.COM


Msikiti wajengwa Kanisani Dar

Na Waandishi Wetu, Desemba 7-13
TUKIO la kipekee zaidi nchini linalogusa vibaya mahusiano kati ya dini ya Kikristo na ya Kiislamu limetokea jijini Dar es Salaam. Tukio hilo ni la Waislamu kununua nyumba iliyokuwa usoni mwa kanisa moja la kilokole na kisha kuamua kujenga msikiti papo hapo, kiasi ambacho mapaa yanaweza hata kugusana.(Angalia pichani ukurasa wa kwanza).

Kanisa hilo la Assemblies of God, Keko, limekuwepo hapo na linatumiwa kwa ibada kwa zaidi ya miaka miwili ingawa ujenzi wake haujakamilika, lakini ujenzi wa msikiti unaokwenda kwa kasi kubwa ya usiku na mchana umeanza kiasi cha majuma mawili hivi yaliyopita.

Msimamizi wa ujenzi huo aliyejitambulisha kwa gazeti hili kwa ufupi tu kama Sheikh Lukinga, aliliambia gazeti hili mwishoni mwa wiki kuwa fedha zinazotumika kujengea msikiti huo zimetolewa na kampuni moja ya mafuta kutoka Uarabuni iliyoko nchini iitwayo Oil-Com.

Sheikh huyo alisema, Oil-Com, ndio waliowanunulia kiwanja katika eneo hilo baada ya wao kupendekeza kuwa wanapapenda zaidi hapo "kanisani" kwani kuko barabarani na pia wanataka kutekeleza alichokiita "agizo la Serikali" kwamba dini zote zisali pamoja kuonyesha umoja na mshikamano.

"Hujasikia Bwana serikali ikisisitiza watu kusali pamoja? Wao (Wakristo) kama wana hofu ni juu yao sisi hatuna cha kukhofia; tutaswali na tunaamini kuwa hakuna mwenye kuweza kutubughudhi," alisema Sheikh Lukinga.

Imamu Lukinga,pia alisema, miaka ishirini iliyopita Waislamu walikuwa na msikiti katika maeneo ya karibu na hapo, lakini Serikali iliuza eneo hilo kwa "kalasinga" mmoja ambaye alitakiwa awalipe fidia wenyeji akashindwa, na ndipo baadaye kampuni ya Oil-Com, ikajitokeza kupanunua na kuwalipa wananchi.

Alisema(Lukinga) kuwa hapo Waislamu, walikataa kupokea fedha taslimu na wakataka wajengewe msikiti, ndipo wakapendekeza wajengewe katika eneo hilo.

"Baada ya wamiliki wa Oil-Com kukubaliana na masharti yetu walitutaka tupendekeze eneo ambalo tunataka tujengewe msikiti mpya na eneo hili lilikuwa na nyumba ya kawaida ambayo tuliinunua na kisha tukapendekeza kujengewa msikiti hapa," alisema Sheikh huyo.

kufuatia ujenzi wa msikiti huo Mchungaji wa Kanisa hilo Paulo Shemsanga, amewatangazia waumini wake kuendesha maombi maalum ya kufunga na kumlilia Mungu aingilie kati hali hiyo. Maombi yalianza rasmi Jumapili iliyopita.

Kwa mujibu wa Waumini wa Kanisa hilo lililopo eneo la Keko Molem, Jumapili iliyopita Mchungaji wao aliwatangazi kuwa nyumba inayojengwa umbali wa kama hatua moja tu kutoka kwenye mlango wa kanisa lao ni msikiti, hivyo waumini wote waendeshe maombi maalum ili kumlilia Mungu kwa kuwa inaonekana kuwa hivyo ni vita vya kiroho.

Nyakati" lilipotembelea kanisani hapo Jumatano na Alhamisi ya wiki iliyopita liliwakuta mafundi wakiendelea kujenga msikiti huo huku baadhi ya kuta zikiwa zimefika usawa wa madirisha na wakisimamiwa na baadhi ya Waislamu waliokuwa wamevalia kanzu na "baraghashia".

Sheikh Lukinga, alisema kuwa iwapo kuna haja ya kundi moja kuhamisha nyumba yao ya ibada, basi Wakristo ndio wafanye hivyo,lakini si wao (Waislamu) kwa kuwa eneo hilo wao wamekuwa wakiswali kwa muda mrefu sana, japo sio hapo hapo wanakojenga sasa.

Nyakati ilipofika nyumbani kwa mchungaji Shemsanga kuzungumzia suala hilo haikumkuta lakini mkewe, Mama Shemsanga, alisema kuwa ni kweli kuwa hali kwa sasa ni ya wasiwasi na Jumapili iliyopita walitangaziwa kuomba ili Mungu aingilie kati.

Alisema kuwa ingawa yeye si msemaji wa kanisa lakini kama muumini ameshuhudia mambo mbalimbali ambayo yanadhihirisha wazi kuwa eneo hilo lina vita ya kiroho na wapo watu wasiopenda wao wasali hapo.

Alisema katika siku za karibuni mmoja wa vijana wa kanisa hilo aliokota karatasi iliyoandikwa maandishi waliyohisi ni ya lugha ya kiarabu na kuwekwa kanisani hapo na hawakujua ni nani kafanya hivyo, ambapo waliyateketeza kwa moto kwa jina la Yesu.

"Si hivyo, tu kwani juzi kuna mmoja wa akinamama wa kanisani ambaye awali alikuwa Muislamu kabla ya kufunuliwa neno na kisha kumpokea Bwana Yesu, alituambia kuwa Waislamu walifika kwa shemeji yake jirani na nyumbani anakoishi wakihoji na kisha kuandikisha majina ya Waislamu wote kwenye eneo hilo kwa kile walichodai kuwa wanahitaji ushirikiano maalum katika kipindi hiki,," alisema Mama Mchungaji, na kuongeza kuwa wanaamini uandikishaji huo ni sehemu ya mapambano hayo ya kiroho.

"Nyakati" liliambiwa kuwa Mchungaji Shemsanga, Alihamisi iliyopita alikuwa amekwenda ofisini kwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, kufuatilia taarifa alizopeleka huko kuhusu ujenzi wa msikiti huo nje ya kanisa.

Hata hivyo, kwa kuwa Mchungaji mwenyewe hakupatikana hadi tunakwenda mitambani, haikuweza kufahamika kuwa alipata jibu gani kuhusu suala hilo ambalo linaonekana kuwa ni jipya katika mitafaruku ya kidini nchini.

Joka laanguka Kanisani na kuleta kizaazaa

Mwandishi Wetu, Desemba 7-13
MOJA ya matukio ya kustaajabisha katika mwaka huu, linaweza kuwa hili la juzi tu ambapo joka moja kubwa lilianguka ghafla kwenye madhabahu ndani ya kanisa wakati mtumishi mmoja alipokuwa akihubiri.

Joka hilo kubwa na la aina yake lilileta tafrani kanisani hapo baada ya kudondoka toka juu ya dari la kanisa wakati Mchungaji Isdori Msekwa akiwa anaendelea na mahubiri.

Tukio hilo lilitokea Jumapili katika Kanisa la Kiinjiri la Kilutheri Tanzania (KKKT), Usharika wa Karanga mjini hapa.

Lakini watu wengi kanisani hapo ambao tayari walishaanza kukimbia kimbia hapa na pale, waliushangaa ujasiri wa mchungaji huyo ambaye pamoja na vitisho vya joka hilo, aliwaambia: "Msihangaike kutoka mwacheni huyu hapo alipo, sisi tuendelee na mahubiri."

Ndipo mahubiri yakaendelea na kufuatiwa na utoaji sadaka na kufunga ibada kama kawaida. v

Wakati wote huo, joka hilo ambalo haikufahamika lilikotokea wala malengo yake, lilikuwa limeduwaa pembeni mwa kanisa hadi ibada Ilipokwisha.

Ndipo baada ya taratibu za ibada kukamilika, na waumini kutoka nje, baadhi yao walirejea ndani na kulikong'oka hadi wakalimaliza papo hapo na kukamata njiti ya kiberiti na kuliwasha moto.

Katika siku za hivi karibuni, kumekuwa na matukio mbalimbali ya vitisho dhidi ya makanisa na wahudumu hata wanapokuwa katika kuhubiri.

Inaaminika kwamba shetani anaendelea na kazi yake ya kuwakatisha tamaa Wakristo lakini nguvu za jina la Yesu zimekuwa zikimdhoofisha na kumteketeza kabisa.

Mgogoro KKKT Mwanga bado mgumu

Na Waandishi wetu,Desemba 7-13
WAKATI suluhisho la mgogoro wa kudai dayosisi mpya ya Mwanga ya KKKT bado ni kitendawili, anayeongoza kundi linalodai dayosisi hiyo mpya, Askofu Abraham Msangi, amemtaka Mwenyekiti wa Tume ya Kutafuta Mwafaka, awape haki yao ya msingi ya kumwabudu Mungu katika makanisa waliyoshiriki kuyajenga kwa kuwa kuwazuia ni kutojali mchango wao.

Askofu Msangi amenukuliwa akisema kuwa wamevumilia kwa muda mrefu kwa kusali nje ya makanisa ambayo walivuja jasho kuyajenga, na sasa imetosha wanataka wapatiwe haki ya kumwabudu Mungu katika mahali panapostahili akimaanisha ndani ya makanisa. A

kihojiwa na kituo kimoja cha redio cha hapa nchini juzi, Askofu Msangi alisema ili kudumisha amani, tume hiyo inayoongozwa na Askofu Mstaafu wa Dayosisi ya Mashariki na Pwani, Elinaza Sendoro haina budi kuharakisha kupanga ratiba ya jinsi makanisa yatakavyotumiwa kwa zamu na pande zote mbili zilizo kwenye mgogoro huo.

"Kwa kuwa kusali ni haki ya kila Mtanzania na kwa kuwa makanisa yaliyopo yalijengwa na makundi yote ya waumini, hakuna haki ya kundi moja pekee kusali na wengine wanyimwe haki hiyo. Huu ni wakati mwafaka wa tume kupanga ratiba ya kuyawezesha makundi yote kusali bila kubughudhiana," alisema askofu huyo.

Kadhalika katika maelezo yake, aliiomba serikali iingilie kati mgogoro huo kwa kuwa ameona kwamba muda unaendelea kwisha na waumini wanateseka nje huku suluhisho likiwa halipatikani na matokeo yake yanaweza kuwa mabaya.

"Watu wamechoka kusali nje, wamechoka kunyeshewa mvua wakati makanisa yao walioyoyajenga yapo; ni vema sasa haki ikapatikana kuliko kusubiri hasira za watu waliochoka," alitahadharisha.

Mgogoro wa Mwanga unasuluhishwa na tume maalum inayoongozwa na Askofu Sendoro ambayo imekuwa ikitafuta suluhu ya mgogoro huo kwa muda mrefu sasa lakini ikikumbana misimamo isiyokubali kubadilika kutoka pande zote mbili.

Upande wa uongozi wa kanisa, unashikilia msimamo wa Mkutano Mkuu wa KKKT, kwamba hakuna dayosisi mpya itakayoanzishwa hadi mwaka 2025, wakati upande wa waumini wa Mwanga wa kanisa hilo wanaodai dayosisi yao, unasema hauwezi kurudi katika dayosisi ya Pare mpaka kanisa liondoe msimamo huo.

Askofu Sendoro hakuweza kupatikana mara moja na wala hajasikika hadi sasa akiyazungumzia madai ya Askofu Msangi.

Mtoto aliyepooza mwaka mzima aponywa na Bwana Yesu

Na Mwandishi wetu, Desemba 7-13
MTOTO Mary Richard Salugole (6), ambaye alikuwa na maradhi ya kupooza kwa zaidi ya mwaka mmoja, amesema umefika wakati ambao wasioamini kuwa Yesu Kristo anaponya, waache ubishi ili wamwendee Yesu kama suluhisho pekee la matatizo yote yakiwemo maradhi.

Katika mazungumzo na mwandishi wa habari hizi yaliyofanyika wiki iliyopita huko Kibamba nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam, mtoto huyo aliwataka wasioamini uponyaji wa kiungu, wapate somo kutokana na uponywaji wake yeye.

Alisema: "Hakuna kitu chochote ambacho kina uwezo wa kushindana na mapenzi ya Mungu na hasa kama mtu ana imani thabiti bila kutetereka na kuacha kumsikiliza Ibilisi anayewatafuta na kuwakatisha tamaa watu wa Mungu."

Kufuatia kuponywa kwa mtoto huyo, baba yake aliamua aandae tafrija ya kumshukuru Mungu na kushuhudia matendo yake makuu kwa familia yao hususan kwa mtoto huyo pekee kwenye familia hiyo, ambayo ilifanyika huko Kibamba nyumbani kwao.

Akiielezea historia ya matatizo ya mtoto huyo, baba yake alisema kwamba ilikuwa siku moja usiku wa saa saba, mtoto huyo aliomba kupelekwa kujisaidia lakini muda mfupi baadaye ghafla alijisikia akiishiwa nguvu maungoni na kushindwa hata kushika kitu au kusimama.

Aliendelea kusema kuwa usiku huo walianza maombi na kulipokucha walimpeleka Hospitali ya Tumbi iliyopo Kibaha mkoani Pwani kwa matibabu.

Mzazi huyo akasema kutokana na imani thabiti ya mtoto huyo kwa Mungu, aliwapa nguvu wazazi wake na hasa alipokuwa akisisitiza mara kwa mara kwamba atapona tu kwa jina la Yesu, kwa hiyo wasiwe na wasiwasi wowote juu ya ugonjwa huo.

Mzazi huyo akasema kwamba hata hivyo baada ya miezi michache, ndipo walipoanza kuona uwepo wa Mungu ukiwashukia huku wakimwona mtoto wao huyo akianza kusogeza mkono ambapo baada ya siku tatu alisogeza mkono wa pili na hatimaye alirudi katika hali yake ya kawaida kabisa. "Mwanangu alikuwa akitusihi tuwe na imani thabiti na kuamini ya kuwa yeye ameshapona kwani alisema kuwa kinywa kikiripo basi tendo hilo hutendeka kama vile kinywa kilivyokiri," alisema baba wa mtoto.

Awali katika tafrija hiyo, baba wa mtoto alisema kwamba aliandaa sadaka maalum katika azma yake ya kuondoa (kutimiza) nadhiri yake kwamba kama mtoto wake atapona maradhi yaliyomsibu, angemtolea Bwana sadaka ya shukurani.

Kwa upande wake mtoto huyo alisema kwa msisitizo: "mimi ninaamini kuwa Yesu Kristo alikufa kwa ajili yetu na kutukomboa kutoka katika shimo la mauti kwa hiyo nina imani ya kuwa shetani asingeweza kunishinda kwa kuwa ninaye Yesu aliyenifia kwa ajili ya ukombozi wangu, shetani ameshindwa."

Mchawi atangaza vita na mchungaji

Na Mwandishi Wetu, Dodoma. Oktoba 19 - 25
VITISHO dhidi ya watenda kazi wa Injili ya Yesu, vinavyofanyika duniani kote, vimeendelea kujitokeza na sasa wala si mbali tena ni hapa hapa nchini kwetu ambapo mchungaji mmoja wa kipentekoste ametishiwa kuuawa eti kwa kuwa anakwamisha biashara ya uchawi kwa kuwahubiria watu Injili hata wakaamua wasikanyage tena kwenye ushirikina.

Mtumishi wa Mungu aliyetishiwa kutolewa roho, ni Mchungaji Amos Mchagalo wa TAG, kijijini Zamahelo, mjini hapa, akidaiwa kwamba anahubiri mno na sasa wateja wanakosekana kutokana na kuhubiri kwake.

Mchungaji huyo ameliambia gazeti hili kwamba mchawi huyo maarufu kijijini hapo (jina linahifadhiwa), ameonya kwamba kwa kuwa sasa watu wengi wanaokoka na kuachana naye, biashara yake itayeyushwa na Injili hali itakayomnyima riziki yake kwa njia hiyo haramu ya kupata riziki.

Mchungaji Mchagalo akasema kwamba kigagula huyo mwenye takriban miaka 70, akishirikiana na mjukuu wake, wamekuwa maarufu kijijini hapo huku wakiendelea kupeleka mkono kinywani kwa kazi yao chafu machoni pa Mungu.

Mchungaji huyo akasema kwamba kutokana na maombi kwa jina la Yesu, mama mmoja aliyefahamika kwa jina la Bibi Marysiana Maweza, ambaye alikuwa na mimba iliyodumu kwa miaka miwili na nusu bila ya kujifungua ingawa alihangaika kwa washirikina wengi kama mchawi huyo, alijifungua mtoto aliyepewa jina la Syliana ambaye ni mzima wa afya. Akasema kwamba inaaminika mimba hiyo ilipigwa juju na wachawi ili mhusika asijifungue kwa wakati upasao.

Baada ya tukio hilo lililomwondolea mzigo na kero za ujauzito, Mama Syliana akaamua aokoke na sasa amejiunga nan kanisa la TAG kijijini hapo. Mchungaji huyo ametoa wito kwa madhehebu mbalimbali ya Kikristo kushirikiana ili kuvunja ngome ya wachawi kijijini hapo.