UKURASA WA MBELE

KAULI YA MHARIRI

MAONI YA MHARIRI

MEI 21, mwaka huu, Mkurugenzi wa Habari wa Ikulu Bw. Peter Kalaghe, alitangaza azimio la Rais Benjamin Mkapa kuunda mtandao wa waandishi wa habari za Ikulu kutoka katika vyombo mbali mbali kwa nia ya kuwa karibu nao na kuwawezesha kuripoti kwa "roho" moja habari za utendaji wa Serikali.

Kalaghe akasema, kuwa waandishi hao watakuwa na mikutano ya mara kwa mara na watendaji wakuu wa Serikali akiwemo Rais ili kufahamu shughuli za Serikali na kujenga uhusiano mzuri kikazi.

Tunapenda kuipongeza hatua hiyo kwa kusema kuwa katika hili Rais Mkapa anastahili pongezi kwani atakuwa amejiwekea historia ya kipekee katika mahusiano na vyombo vya habari ambavyo ni mhimili wa nne katika uendeshaji wa nchi.

Lakini jambo moja la kusikitisha ni kwamba kumekuwa na utamaduni ndani ya Serikali kwa muda mrefu wa kuvibagua vyombo vya habari vya kidini, bila kujua kuwa navyo vina jamii vinayoihudumia ambayo ni sehemu ya Watanzania. Ikulu haikuvishirikisha vyombo vya habari vya kidini katika mpango huu.

Ni jambo la kusikitisha kuona kwamba viongozi wengi wa Serikali hawajui kuwa vyombo hivi vya kidini vina wateja (audience) wengi na baadhi yake vikivizidi vyombo vingine mseto (circular) kwa umbali mkubwa tu.

Mbali ya hayo vyombo hivi vina kiwango cha juu cha ushawishi katika jamii, bila shaka kuliko vile inavyodhaniwa na baadhi ya watendaji wa Serikali.

Kumekuwa na utamaduni wa kuvinyima matangazo vyombo vya habari vya kidini na kutovishirikisha katika masuala na mialiko mingi hata ile inayohusu mambo ya dini.

Bila shaka Watendaji wa Serikali wamemezwa na dhana potofu kuwa kwa vile Serikali yetu haina dini, basi haifai pia kushirikiana na vyombo vya habari vya kidini. Au kwa vile baadhi ya vyombo vimekuwa vikiishambulia Serikali, basi inafaa kuviepuka kabisa vyombo vyote.

Sisi tunaamini kuwa hata vile vyombo vinavyodhaniwa kuwa vina chuki au vina sera ya kuishambulia Serikali, vinahitaji ushirikiano zaidi kuliko kutengwa. Kwamba mradi tu vyombo hivi licha ya kutokuwa na matangazo vinaendelea kuwepo na vikiwa na wasomaji wengi ni ishara ya kwamba vinakubalika katika jamii na vina ushawishi kwa idadi kubwa ya Watanzania.

Tuonavyo sisi ni kwamba njia nzuri ya kuifahamu jamii inayohudumiwa na vyombo hivyo ni kuvisaidia vyombo hivyo viendelee kuwepo na njia nzuri ya kuvifanya viwe vya manufaa kwa jamii nzima ni kushirikiana navyo kwani kuvitenga kunaongeza ufa kati ya jamii vinayoihudumia na Serikali kuliko kuupunguza ufa huo. Tunaamini kwa kusoma katikati ya mistari hii mtu mwenye hekima anaweza kuelewa vizuri kila tunachomaanisha.

Copyright © 2002-2003 Nyakati
Email the Webmaster